Waombaji kazi watakiwa kuthibitisha nyaraka zao na kuzihuisha kwenye mfumo wa Ajira.
utumishi |
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Bw. Xavier Daudi amesema hayo wakati akiongea na Waandishi wa Habari ofisini kwake waliotaka kufahamu juu ya maboresho yaliyofanyika katika Mfumo huo wa maombi ya kazi unaopatikana kwa anuani yaportal.ajira.go.tz
Daudi amesema kuwa Ofisi yake ilimepewa dhamana ya kutafuta rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma imekuwa ikitumia kila njia kuhakikisha Serikali inapata Watumishi wenye sifa, weledi na maadili mema huku ikihakikisha wadau wake wanapata huduma bora kulingana na wakati.
“Kama mnavyofahamu kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo duniani hususan matumizi ya teknolojia, ili kuweza kuendana na kasi hiyo Utumishi wa Umma nchini umekuwa ukifanyiwa maboresho ya mara kwa mara kuanzia miaka 1990 kwa lengo la kukidhi matarajio ya wadau, ikiwemo utoaji wa huduma bora kwa wakati, sisi kama watendaji wenye dhamana ya kuendesha mchakato wa Ajira serikalini tumekuwa tukiboresha mifumo yetu ya kiutendaji ikiwemo matumizi makubwa kupitia teknolojia ya habari na mawasiliano” alieleza Daudi.
Alifafanua kuwa matumizi ya TEHAMA katika Ofisi hiyo imewasaidia kuwafikia wadau wengi ndani na nje ya nchi kwa muda mfupi, Mfano, hivi sasa mwombaji kazi aliyejisajili katika mfumo wao anaweza kupata taarifa ya uwepo wa nafasi ya kazi, kuitwa kwenye usaili au kupata taarifa ya hatua mchakato ulikofikia kwa ujumbe mfupi kwenye simu yake ya kiganjani au kupitia barua pepe kulingana na njia aliyochagua mdau huyo.
Ameongeza kuwa Sekretarieti ya Ajira imejipanga ndani ya kipindi kifupi kuanzia sasa kuendesha usaili kupitia “video conference”, mfano Wajumbe wa jopo la usaili wanaweza kuwa Dodoma na Msailiwa akawa Zanzibar ambapo sio lazima msailiwa aende Dodoma kwa ajili ya usaili bali anaweza kufanyiwa usaili hukohuko Zanzibar kwa kutumia mtandao wa ‘Internet’.
“Mtaweza kuona tumefikia hatua ya kutaka kuendesha saili kupitia (Video Conference) kutokana na Serikali yetu ilivyoweza kuhakikisha karibu kila eneo katika nchi yetu linakuwa na miundombinu ya mawasiliano, hivyo na taasisi yetu inaona ni wakati muafaka kuendelea kutumia mbinu za kisasa ili kuweza kupima uwezo wa msailiwa badala ya kutegemea vyeti peke yake ikiwa pia ni sehemu ya kusogeza huduma karibu na wadau kwa lengo la kuwapunguzia gharama waombaji kazi”.
Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Kitengo cha TEHAMA katika Sekretarieti ya Ajira Mhandisi Samwel Tanguye alibainisha kuwa mfumo wa maombi ya kazi ‘Recruitment Portal’ umefanyiwa maboresho katika maeneo matatu ambayo ni eneo la taarifa binafsi, taarifa za anuani na taarifa za kielimu.
Aliongeza kuwa waombaji wa fursa za Ajira wanapaswa kuzingatia kuwa endapo wataingiza taarifa zisizo sahihi mfumo utawazuia kuomba kazi wanayoitaka kwa kuwa maboresho hayo yaliyofanyika yamesababisha mfumo kufanya yafuatayo. Mfumo haumruhusu mwombaji kazi mwenye elimu ngazi ya astashahada kuomba kazi ambazo zinawahusu wenye shahada. Vivyo hivyo, mwenye shahada hawezi kuomba kazi zinazowahusu wenye stashahada. Pia, Mfumo una uwezo wa kuwachuja waombaji kazi kulingana na sifa za msingi zilizotolewa katika tangazo. Mfano, endapo moja ya sifa ni umri ama uzoefu, mfumo utawaruhusu wale wenye sifa stahiki.
Pia, endapo tangazo linahusu “professionals”, basi wasio na “professional” hiyo hawataweza kuomba. Mfano, kama tangazo linawataka wahasibu wenye CPA, basi wale wote ambao hawana CPA hawataweza kuomba kazi hiyo.
Mhandisi Tanguye amebainisha kuwa, hivi sasa Mfumo unaweza kumruhusu mwombaji kazi ambaye amepoteza vyeti vyake na hakuwa na nakala za vyeti husika kuomba nafasi za Ajira pasipo usumbufu. Kinachotakiwa kufanya baada ya upotevu wa cheti/vyeti husika ni kutoa taarifa Baraza la Mitihani na Sekretarieti ya Ajira kupata uthibitisho wa elimu yake kutoka taasisi husika (NECTA na Vyuo vingine.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma 30 Mei, 2018 Orinal post from http://www.ajira.go.tz/index.php/news/view/149
EmoticonEmoticon